Jambo la 4 kati ya “Mambo unayohitaji kuyajua kuhusu ndoto unazoota ili iwe vyepesi kufanikiwa kimaisha” ni hili:
“Ikiwa umeota ndoto ambayo tafsiri yake huijui ufanyeje?”
1. OMBA MUNGU AKUPE UFAHAMU JUU YA NDOTO! UFAHAMU HUU JUU YA NDOTO, UKIUPATA TOKA KWA MUNGU KATIKA KRISTO YESU, UTAKUSAIDIA WEWE NA WATU WENGINE PIA!
Biblia inatueleza ya kuwa: “Danieli naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto” (Daniel 1:17).
Kufuatana na Wakolosai 1:9, Mtume Paulo akiongozwa na Roho Mtakatifu aliwaombea wakristo waliokuwepo Kolosai wakati ule, wajazwe “maarifa ya mapenzi yake katika hekima yote na ufahamu wa rohoni”.
Naamini hata katika nyakati za sasa, Roho Mtakatifu yupo tayari kutuongoza tujazwe “ufahamu wa rohoni”. Naamini ufahamu huu wa rohoni unahusu pia ufahamu juu ya ndoto!
2. USITAFUTE TAFSIRI YA NDOTO TOKA KWA MTU YE YOTE TU UNAYEDHANI ANAWEZA KUKUSAIDIA!
Kitabu cha Mwanzo 40:8 tunasoma swali hili: “Kufasiri si kazi ya Mungu” Hayo yalikuwa maneno ya Yusufu akiwahakikishia “Mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri”, juu ya upatikanaji wa tafsiri juu ya ndoto walizokuwa wameota!
Farao alipoota ndoto zake mbili mfululizo zilizofanana, tena kwa usiku mmoja (Mwanzo 41:1 – 7), alitafuta tafsiri ya ndoto zile mahali ambapo hakutakiwa kutafuta!
Farao alitafuta wapi kwanza juu ya tafsiri zake za ndoto alizoota usiku ule? Biblia inasema: “Farao akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko…akawahadithia ndoto zake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria…” (Mwanzo 41:8).
Ni mpaka alipotafutwa Yusufu aliyekuwa gerezani wakati ule, ili amtafsirie Farao ndoto zake. Yusufu akamwambia Farao: “Si mimi, Mungu atampa Farao majibu ya amani” (Mwanzo 41:16).
Ni wazi ufahamu aliokuwa nao Yusufu juu ya ndoto, ulikuwa mkubwa kuliko wa waganga na wachawi wote waliokuwa nchini Misri wakati ule!
Mfalme Nebukadreza aliona jambo kama hili kwa Danieli, alipomlinganisha na waganga na wachawi waliokuwa kwenye himaya yake alipokuwa anatawala.
Biblia inatueleza ya kuwa: “Danieli…alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto” na alifaa “mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake” (Danieli 1:17,20).
Ni kweli kuna mtu ambaye anaweza kukupa tafsiri ya ndoto yako, lakini asiweze kukupa ujumbe uliomo katika ndoto hiyo! Kupewa tafsiri ya ndoto, bila kupewa ujumbe unaoambatana na ndoto hiyo; ni sawa na kula chakula na ukashiba huku hakina virutubisho kwa afya yako.
3. OMBA MUNGU AKUPE KUJUA UJUMBE ULIOMO KWENYE NDOTO ULIYOOTA, ILI USIISHIE KUPATA TAFSIRI YA NDOTO BILA KUJUA UJUMBE WAKE!
Ukisoma kitabu cha Danieli 4:4 – 18, utaona ya kuwa kiu aliyokuwa nayo mfalme Nebukadreza, ilikuwa ni kujua tafsiri ya ndoto aliyoota, na si ujumbe uliokuwa ndani ya ndoto kwa ajili yake!
Lakini Danieli alimpa mfalme Nebukadreza vyote viwili – tafsiri ya ndoto (Danieli 4:20 – 26), na ujumbe uliokuwemo kwenye ndoto ile kwa ajili yake (Danieli 4:27).
Na kwa sababu mfalme Nebukadreza alitaka tafsiri ya ndoto, na si ujumbe wa ndoto, alijikuta akipuuzia na kutokutilia maanani ujumbe wa ndoto aliopewa, wala hakuufuatilia! Na matokeo yake ni maisha ya mateso ya miaka saba, kwa ajili yake, na kwa ajili ya familia yake, na kwa ajili ya serikali ya ufalme wake.
Unapoendelea kutafakari juu ya jambo hili, ni vizuri nikujulishe pia yafuatayo:
(i) Kuna ndoto ambazo zimebeba vitu vinavyohitaji tafsiri ili uweze kupata ujumbe uliomo ndani yake. Mfano wa ndoto kama hizi tunaupata katika Mwanzo 40:5 – 23
(ii) Kuna ndoto ambazo zimebeba vitu ambavyo maana yake iko wazi, na kwa ajili hiyo havihitaji tafsiri yake, ili kuupata ujumbe uliomo ndani yake. Soma mfano wake katika Mathayo 1:18 – 24.
(iii) Kuna ndoto ambazo zina ujumbe peke yake, bila kubeba vitu vyovyote zaidi ndani yake. Soma mfano wake katika Mathayo 2:12,22 na Mwanzo 31:24,29.
(iv) Mfasiri sahihi wa ndoto na ujumbe uliomo ndani yake ni Mungu tunayemwabudu katika Kristo Yesu; bila kujali chanzo cha ndoto uliyoota!
4. UWE NA NENO LA BIBLIA LA KUTOSHA NDANI YAKO – TENA KATIKA HEKIMA YOTE!
Wakolosai 3:16 inasema hivi: “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana…”
Kwa nini jambo hili ni la muhimu katika kutafsiri ndoto na kupata ujumbe uliomo ndani yake? Hii ni kwa sababu kufuatana na Ayubu 33:14,15 – ndoto ni neno katika picha!
Na kwa kuwa “kusikia huja kwa neno la Kristo” (Warumi 10:17), basi ujue bila neno la Kristo ndani yako huwezi “kusikia” ujumbe uliomo ndani ya ndoto – hata kama unajua tafsiri ya ndoto hiyo!
Hebu tuangalie mfano juu ya Biblia inasema nini kuhusu tafsiri ya ndoto zinazohusu madarasa, au kusoma, au kufanya mitihani; na ujumbe uliomo ndani yake.
Ukisoma kitabu cha Danieli 1: 3 – 20 unaweza kujifunza yafuatayo juu ya ndoto hizo:
(i) Maandalizi yanahitajika kwa ajili ya hatua iliyo mbele yako, au hatua unayotaka Mungu akupe unapoomba katika maombi yako.
(ii) Kuota “shule” au “chuo” maana yake maandalizi ya hatua fulani iliyo mbele yako yanahitaji utaratibu maalumu.
(iii) Kuota “shule” au “chuo” ulichowahi kusoma zamani, ina maana kwamba kuna jambo lililotokea hapo ulilotakiwa “kuvuka” – lakini hukuweza kuvuka, na kwa hiyo kuna eneo limekwama kwenye maisha yako.
(iv) Watu mlio nao darasani katika ndoto ina maana watu mlio ngazi moja ya kimaandalizi(v) Kuota ndoto uko darasani na watu uliowahi kusoma nao zamani au unaota unarudia darasa, au unarudia mtihani – ina maana umekwama mahali kimaisha na unahitaji maandalizi ili kuvuka hapo.
(vi) Ukiota hukai darasani wakati wengine wako darasani; au hukai kwenye mtihani wakati wengine wanafanya mitihani – ina maana huna utulivu unaotakiwa uwe nao ili uweze kujiandaa vyema kwa hatua iliyo mbele yako.
(vii) Ukiota unafanya mtihani – ujue: au unapita mahali kimaisha ambapo unapimwa kiwango chako ulichofikia kimaandalizi; au mbele yako kuna kuja kipimo kwa ajili ya kujua ikiwa umefikia kiwango kinachotakiwa kwa wewe kuingizwa hatua nyingine ya maisha
(viii) Ukiota unaota unasoma, na ukaona na somo unalosoma, au ukaota unafanya mtihani na ukaona somo la mtihani huo – ina maana unaonyeshwa aina ya, au eneo la – maandalizi unalotakiwa kulifuatilia kimaandalizi
Kumbuka – huu ni mfano tu wa kutafsiri ndoto na kupata ujumbe uliomo ndani yake kwa kutumia neno la biblia.
Mungu aendelee kukubariki unapoendelea kujifunza somo hili la ndoto.
No comments:
Post a Comment