Jambo la 5 kati ya “Mambo unayohitaji kuyajua kuhusu ndoto unazoota ili iwe vyepesi kufanikiwa kimaisha” ni hili hapa:
“Omba Mungu akupe kujua muda uliomo katika ndoto, unaokupa kuomba na kujiandaa, au kubadili kuhusu uliyoota”.
Si ndoto zote zina kipengele cha “muda” wa namna hii, ingawa nyingi zinao, lakini wengi wanashindwa kuufuatilia!
Hebu tujifunze jambo hili kwa mifano ifuatayo:
Mfano wa 1: NDOTO ZA FARAO
Habari za ndoto hizi tunazipata tunaposoma Mwanzo 41:1 – 36. Ndoto zote mbili alizoota Farao katika usiku mmoja, zilikuwa na msisitizo mkubwa uliowekwa kwenye “muda”!
• Ndoto zote zilikuwa na matukio ya jumla ya “muda” wa miaka 14.
• Miaka 7 ya shibe ilihitajika kwa ajili ya kujiandaa, kwa ajili ya miaka 7 ya njaa.
• Sehemu ya 5 ya mavuno ya mwaka mmoja (1) wa shibe, ilihitajika kwa ajili ya mahitaji ya chakula ya mwaka mmoja (1) mzima wa njaa
• Maarifa yalihitajika kwa ajili ya kukusanya mavuno ya kila mwaka katika miaka 7 ya shibe; ili kupata na kutenga, na kulinda sehemu ya 5 kama akiba katika miji.
• Yusufu aliamua kutokuwa “mvivu” wa kuweka akiba kila mwaka. Kwa hiyo akaweka akiba ya chakula, kwa miaka 7 mfululizo, kwa ajili ya miaka 7 ya njaa iliyofuata.
• Wananchi wa Misri hawakuweka akiba ya nafaka bali waliweka akiba ya fedha na wanyama pekee – tena ya kutosha mwaka mmoja (1) tu. Mwaka wa 2 wa njaa walijiuza wao na ardhi yao kwa Farao ili kupata msaada ili wasife njaa.
Kumbuka: Ndoto zote mbili za Farao zilikuwa na msisitizo uliowekwa kwenye “muda”! Bila msisitizo huo wa muda, ujumbe uliokuwa kwenye ndoto zile, usingekuwa wa msaada kwa aliyeoteshwa ndoto!
Mfano wa 2: NDOTO ZA WAFANYAKAZI WA FARAO
Wafanyakazi hawa wawili wa Farao – mmoja alikuwa mkuu wa wanyweshaji na mwingine alikuwa mkuu wa waokaji. Biblia inasema "wakaota ndoto wote wawili kila mtu ndoto yake usiku mmoja, kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake…"(Mwanzo 40:5).
Yusufu aliyekuwa amefungwa nao gerezani – aliwapa tafsiri za ndoto zao…na kukuta zilikuwa na kipengele cha “muda”, kilichofanana katika ndoto zote mbili – za wale wafanyakazi wawili wa Farao!
Muda uliokuwepo kwenye ndoto zao ni “siku tatu” (Mwanzo 40:12,18) – zilikuwa na matukio mawili yaliyokuwa yatokee kwao “siku tatu” baada ya kuota ndoto zao!
Biblia inatupa habari ya kuwa “Ikawa siku ya tatu …Farao…akampandisha mkuu wa wanyweshaji katika kazi yake….Bali akamtundika mkuu wa waokaji, kama Yusufu alivyowafasiria” (Mwanzo 40:20 – 22).
Ndoto zile ziliwapa wahusika ujumbe wa kuwa kila mmoja wao alikuwa na “siku tatu” kabla ya matukio yaliyokuwa kwenye ndoto zile kutokea katika maisha yao!
Swali la msingi la kujiuliza ni kwa nini walipewa muda huo – ikiwa si kwamba walitakiwa kuzitumia kuhusiana na ujumbe uliokuwemo kwenye ndoto zile?
Mfano wa 3: NDOTO YA MKE WA PILATO
Kufuatana na Mathayo 28:19 – ndoto aliyoota mke wa Pilato, ilikuwa imebeba “muda” uliokuwa wa “usiku mmoja”, kama onyo na angalizo kwa mume wake, juu ya ushiriki wake katika maamuzi ya hukumu juu ya Yesu, iliyokuwa ifanyike kesho yake
Ni dhahiri familia ile ya Pilato ilishindwa kuutumia vizuri ule “muda” waliopewa katika ndoto ile!
Mfano wa 4: NDOTO YA NEBUKADREZA.
Hii ni ndoto tunayoipata katika Danieli 4:1 – 37. Ndani ya ndoto hii kulikuwa na “muda” wa aina mbili – na wenye kazi mbili tofauti.
“Muda” wa kwanza – na uliokuwa wazi, ni ule wa kipindi cha “adhabu” ya “nyakati 7” (Danieli 4:16, 23, 24), uliokuwa umekusudiwa kwa Nebukadreza – ikiwa hatabadili tabia zake.
“Muda” wa pili – na ambao haukuwa dhahiri sana, ni ule wa kipindi cha kuangalia ikiwa atafuata ushauri aliopewa – ili adhabu aliyopangiwa isimpate!
Danieli alimpa Nebukadreza ushauri huu: “Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kuwahurumia maskini, huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha” (Danieli 4:27).
Kufuatana na Danieli 4:28, mfalme Nebukadreza alipewa “miezi kumi na miwili” ili kufuata na kutekeleza ushauri wa Danieli. Lakini hakuufuata – na matokeo yake ni kuipata adhabu aliyoona imepangwa kwa ajili yake kwenye ndoto!
Pamoja na kwamba ndani ya ndoto hatujaona miezi 12 hiyo moja kwa moja – lakini ina maana ndoto ile iliendelea kukaa mawazoni mwake kwa mfululizo wa miezi kumi na mbili …ili asiipuuzie – lakini akaipuuzia!
Nakuombea ili Mungu akusaidie, ili ikiwa utaota ndoto yenye “muda” ndani yake – usije ukafanya kosa kama la mfalme Nebukadreza la kutojali ushauri ambao angeutekeleza – angeepuka adhabu iliyokuwa kwenye ndoto ile!
Mungu aendelee kukupa nafasi ya kulifuatilia somo hili kwa umakini kwa kadri ninavyokufundisha! Ni kila siku hapa hapa kuanzia saa 12::00 jioni na kuendelea.
KUNA MAMBO 11 USIYOYAFAHAMU KUHUSU DKT. SHIKA.
ReplyDeleteBonyeza hapa >>> https://goo.gl/6xhHk8 kuyafahamu sasa.